Aliyekuwa Kiungo wa Klabu ya Chelsea Cesc Frabregas anaamini Klabu hiyo itarudi kwa kishindo na kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu England msimu ujao 2023/24.
Chelsea kwa sasa inapitia kipindi kigumu msimu huu ambao umetajwa kuwa ni mbovu kuwahi kutokea katika historia ya klabu hiyo, lakini Fabregas anaamini mambo yatakuwa sawa.
Zikiwa zimebaki mechi nne ligi imalizike, Chelsea ipo katika hatari kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kutokana na kutopata matokeo mazuri licha ya kumtimua Graham Potter.
Kwa sasa Meneja wa mpito Frank Lampard ana presha kubwa baada ya kufungwa mechi sita mfululizo tangu alipoteuliwa mapema mwezi Machi.
Lakini, Fabregas anaamini Chelsea bado haijapoteza mwelekeo na msimu ujao itarudi kivingine kwa hiyo ni suala la muda tu.
Fabregas aliyewahi kubeba ubingwa wa Ligi akiwa na Chelsea mwaka 2017, alizungumza kupitia kituo cha Sky Sports kuhusu mwenendo wa klabu hiyo.
“Miaka sita iliyopita tuliwahi kupitia kipidi kigumu kama hiki, tulimaliza msimu nafasi ya 10 kwahiyo sishangai, Jose Mourinho aliondoka, Guus Hiddink akaja, akaanza kuchezesha wachezaji makinda kama Ruben Loftus Cheek na Tammy Abraham awape uzoefu, nakumbuka baadae Antonio Conte alijiunga na akatufuata kuzungumza na sisi kwenye mazoezi ya timu, lengo atufahamishe mipango yake kuhusu klabu, naamini atapatikana kocha mwenye malengo mazuri na kila kitu kitarudi kwenye mstari,” amesema Fabregas.