Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limeifuta nchi ya Chad kwenye ushiriki wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika 2021, kufuatia misuguano iliopo kati ya serikali ya nchi hiyo na Shirikisho la soka.
Kikosi cha timu ya taifa ya Chad tayari kilikua kimeshaanza kambi ya kujiandaa na mchezo wa mzunguuko wa tano ambao ungewakutanisha dhidi ya Namibia kesho Jumatano (Machi 24) na baadaye kucheza mchezo wa mzunguuko wa sita dhidi ya Mali siku ya Jumapili (Macho 28).
CAF imejiridhisha uwepo wa misuguano kati ya Wizara ya Michezo ya Chad na Shirikisho la Soka, hali ambayo imepelekea kufungwa kwa ofisi za shirikisho hilo mjini Ndjamena tangu Machi 10.
CAF imetumia vifungu vya 61 na 64 vya kanuni zake, na kwa utaratibu huo Chad itakua imepoteza michezo yote miwili dhidi ya Namibia na Mali.
Kabla ya kufutwa kushiriki michezo hiyo ya kuwania kufuzu fainali za Afrika 2021, Chad ilikuwa mkiani mwa msimamo wa Kundi A nyuma ya vinara Mali, ambao tayari wameshafuzu kwa kufikisha alama 10 na wakifuatiwa na Guinea wenye alama 8 na Namibia ina alama 3.