Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa iwapo jambo lolote litatokea kufuatia afya ya Halima Mdee, jeshi la Polisi litawajibika kwa wananchi wake
Hayo yamesemwa na CHADEMA kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano ya Mambo ya Nje, John Mrema, na kueleza kuwa iwapo afya ya Halima Mdee ambaye ametoka kufanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini, ikitetereka kwa namna yoyote ile, basi itawajibika juu ya hilo.
Sambamba na hilo CHADEMA wametoa wito wa kumpatia dhamana mbunge huyo, ambaye mpaka sasa anashikiliwa na jeshi la polisi katika kituo cha kati jijini Dar es salaam.
“Tunasikitishwa na kulaani kitendo hiki cha polisi kuendelea kumshikilia mgonjwa ambaye alikuwa amelazwa hospitalini. Jeshi la Polisi litawajibika kwa watanzania endapo afya ya Mhe. Halima Mdee ikitetereka au ikidhoofu zaidi na lawama zote. Tunatoa mwito kwa Jeshi la Polisi limpatie dhamana ili aweze kuendelea na matibabu yake, kwani dhamana ni haki yake na zaidi ni kuwa huyu bado ni mtuhumiwa na ni Mgonjwa ambaye ametoka hospitalini”, imesema Taarifa hiyo.
Hata hivyo, Mdee alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Mwl. Nyerere jijini Dar es salaam akitokea Afrika Kusini, alikokuwa akipatiwa matibabu.