Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini kimelalamikia kitendo cha mawaziri kujitokeza na kufanya kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Monduli na kueleza kuwa kitawafikisha kwenye kamati ya maadili ya taifa.

Hayo yamesemwa na katibu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini ambaye pia ni mwenyekiti wa chama mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, ambapo amesema kuwa mbali na malalamiko yao ya kutotendewa haki katika uchaguzi uliofanyika, lakini watawashtaki mawaziri waliopiga kampeni.

“Sisi kama viongozi tulijipanga vyema kuanzia kampeni tumeona uvunjivu wa sheria mwingi na tumerekodi kila kitu ikiwemo mawaziri kuja kufanya kampeni huku wakiahidi utekelezaji wa miradi kitu ambacho ni kinyume na sheria ya uchaguzi hivyo tutawafikisha kwenye kamati ya taifa ya maadili,” amesema Golugwa

Aidha, Golugwa amewataja baadhi ya mawaziri waliofika jimboni Monduli wakati wa kampeni na kutoa ahadi ni pamoja na waziri wa Ardhi, William Lukuvi, Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso, pamoja na Naibu waziri wa Madini, Doto Mashaka Biteko.

Hata hivyo, amefafanua kuwa katika kipindi hicho cha kampeni walishuhudia mawaziri hao wakitoa ahadi na kufanya baadhi ya mambo ambayo kimsingi yapo kinyume na sheria na taratibu za uchaguzi.

 

Video: Polepole afichua siri ya ushindi CCM, amshukia Makonda
CAF yamtangaza 'Pilato' wa Cape Verde Vs Tanzania