Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepanga kufanya tukio la aina yake la kumkabidhi kadi mwanachama wake mpya, Wema Sepetu aliyetangaza kujinga na chama hicho akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Habari wa Chadema, Tumaini Makene jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na mwandishi wa habari wa Mtanzania.
“Wema atakabidhiwa kadi kwa utaratibu maalum maana ameonesha heshima na nia ya kujiunga kwenye mapambano ya kweli,” Makene anakariwa, ambapo aliongeza kuwa ujio wa mrimbwende huyo ni faraja kwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini kwani anaingia na timu kubwa ya watu wanaomuunga mkono.
“Tena na wengine wanatoka katika mashirika mbalimbali ikiwemo TFF. Kwa hiyo hapa unapata picha Wema ni mwanachama wa Chadema mwenye mvuto wa aina yake na huwezi kubeza hata kidogo kuja kwake,” aliongeza.
Makene alifafanua kuwa tukio hilo maalum limepangwa kufanyika kabla ya Machi 5 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Alisema siku huyo zaidi ya watu 500 wanaomuunga mkono Wema watajinga na Chadema.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Wema ambaye katika uchaguzi mkuu uliopita aliongoza kampeni ya ‘Mama Ongea na Mwanao’ akiwa katika timu ya mgombea mwenza wa CCM ambaye sasa ni Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu, akiongozana na mama yake walifanya mkutano na waandishi wa habari na kutangaza kujiunga rasmi na Chadema.
Alidai kuwa amechukua uamuzi huo kwa hiari kwa lengo la kupigania demokrasia na kwamba anaamini lengo lake litatimia kupitia chama hicho kikuu cha upinzani.
Wikendi hii, Wema alionekana akiwa katika uwanja wa Taifa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuangalia mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga. Hii ilikuwa mara ya pili wawili hao kuonekana pamoja baada ya kuongozana Mahakama Kuu kusikiliza kesi iliyofunguliwa na Mbowe dhidi Kamanda wa Polisi wa Dar es Salaam, Simon Sirro, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi hilo ambapo alitakiwa kumuongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Uamuzi huo wa Wema ulikuja siku chache baada ya kutoka selo za polisi alikokuwa akishikiliwa baada ya kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kati ya orodha ya watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya na watumiaji wa dawa za kulevya. Wema aliyeshikiliwa kwa siku takribani 7 katika selo za polisi anakabiliwa na kesi ya matumizi ya dawa za kulevya.
Akikanusha tuhuma hizo dhidi yake, alionesha kutopendezwa na utaratibu uliotumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kumuita kupitia vyombo vya habari akimhusisha na tuhuma za dawa za kulevya.