Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika amesema hawatoshiriki mchakato wa kutoa maoni mbele ya kikosi kazi kama ilivyoratibiwa na Msajili wa vyama vya siasa.
Mnyika ameyasema hayo leo Mei 23, 2022 wakati akizungumza na vyombo vya Habari na kuongeza kuwa ratiba hiyo iliyotolewa Mei 20, 2022 mbali na mambo mengine inaonesha CHADEMA itatoa maoni yake Mei 24, 2022.
“Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa tarehe 20 mwezi huu ilitoa ratiba kwa umma na inaonesha kesho jumanne tar 24 CHADEMA itatoa maoni yake mbele ya kikosi kazi nipende kutoa msimamo wa chama kuwa hatutoshiriki mchatako huo”
Kwa mujibu wa Mnyika amesema ofisi ya Msajili imepandikiza migogoro kwenye vyama takribani vitano hivyo anatoa wito kwa mamlaka husika kuchunguza mwenendo wa ofisi hiyo na kisha kuchukua hatua.
Katika hatua nyingine Mnyika amesema uamuzi wa CHADEMA kushiriki mazungumzo na Rais Samia una baraka za Kamati kuu na Baraza Kuu lakini hawazuii maoni na mitazamo tofauti ya Wanachama wao.
“Ipo shauku ya baadhi ya Wanachama kutaka kujua ni mambo gani yanayoendelea na kama hawa waliotufanyia yote haya leo hii tunakaa nao ni kweli wana jambo jema? tuvute subira” amefafanua Mnyika.
Aidha amefafanua kuwa mazungumzo hayo yamefuatiwa na hatua za awali na si kama wengi wao wanavyodhani na kwamba wana CHADEMA na Watanzania wanatakiwa kuwa watulivu kwani mchakato wa mazungumzo, kujenga maridhiano na mwafaka sio tukio la siku moja.
“Hatma ya nchi hii haiko kwa CCM na CHADEMA pekee hususani katika suala muhimu kama katiba nitoe rai kwa Watanzania kuwa watulivu na umma utashirikishwa lengo ni kupata katiba mpya ikifika mwaka 2025,” amesisitiza.
Mei 20, 2022 viongozi wakuu wa CHADEMA walishiriki kikao cha majadiliano na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe, Makamu mwenyekiti Zanzibar Saidi Issa Mohamed, Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati kuu na Sekretarieti ya chama hicho.