Wakati nyasi za uwanja wa kampeni wa jimbo la Monduli zikisubiri kushika joto kali la msuguano wa hoja kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge, tayari sauti za kilio cha ‘rafu’ zimeanza kusikika.
Chadema ambao wanatetea jimbo hilo baada ya aliyekuwa mbunge wake, Julius Kalanga kujiuzulu na kuhamia CCM ambako anagombea tena nafasi hiyo wamedai kuwa wanafahamu mbinu za uchakachuaji zinazopangawa na wapinzani wao.
Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, Aman Golugwa amesema kuwa wamebaini mbinu za kucheza rafu zinazopikwa na CCM ikishirikiana na vyombo vingine kwa lengo la kuchakachua lakini wamejipanga kuionesha dunia kuwa CCM haikubaliki Monduli.
Amesema kuwa katika uzinduzi wa kampeni utakaofanyika Jumatano eneo la Mto wa Mbu, viongozi mbalimbali waandamizi wa chama hicho watahudhuria ikiwa ni pamoja na waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa takribani miaka 20.
Aidha, kwa upande wa CCM wao pia wamejipanga kuanza kampeni kwa kishindo ambapo katika siku hiyohiyo watafanya uzinduzi Monduli mjini.
Kalanga amesema kuwa wamejipanga kuzindua kwa kishindo kampeni za uchaguzi huo ambapo Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula ataongoza uzinduzi huo.
“Tutazindua kampeni zetu Jumatano. Nina uhakika kuwa tutashinda kwa sababu CCM ina nguvu kubwa na inakubalika sana Monduli,” alisema Kalanga.
Katibu wa Uenezi wa CCM mkoa wa Arusha, Shaban Mdoe alitoa wito kwa wafuasi wa CCM monduli kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi huo wa kampeni kuonesha mshikamano wao.