Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea kuonesha kukaidi katazo la Serikali kuhusu uamuzi wao wa kuendesha oparesheni UKUTA Septemba 1 mwaka huu, ambapo wameanza kusambaza bendera maalum za operesheni hiyo.

Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Casimir Mabina amesema kuwa wameamua kugawa bendera hizo kama sehemu ya kuonesha uungwaji mkono wa operesheni ya chama hicho.

Alisema kuwa wafuasi wa chama hicho wanaweza kupeperusha bendera hizo kwenye magari, ofisi, maduka na hata nyumba zao.

“Mwenye gari aweke bendera, mwenye ofisi, mwenye duka, kila kona Tanzania tandazeni bendera za chama kama kama ishara ya kuunga mkono uamuzi wa chama chetu wa kupinga uminywaji wa demokrasia unaofanywa na Serikali ya awamu ya tano,” alisema Mabina alipozungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mbina ameeleza kuwa ingawa Rais Magufuli alipiga marufuku siasa za chama hadi mwaka 2020, yeye amefanya ziara ambayo imeanzia makao makuu ya CCM, Chamwino Dodoma akinadi chama hicho na kwamba jana alihimitisha katika ofisi ndogo za CCM zilizoko Lumumba jijini Dar es Salaam.

Kamati Kuu ya Chadema iliamua kufanya maandamano na mikutano nchi nzima Septemba 1 mwaka huu wakidai kuwa hiyo ni haki yao kikatiba. Chama hicho kinapinga agizo la Rais Magufuli kuzuia mikutano ya kisiasa kwa watu ambao hawakuchaguliwa kwenye uchaguzi uliopita.

Rais Magufuli amepiga marufuku maandamano hayo akiwataka Chadema kutomjaribu kwani yeye ni wa tofauti na hajaribiwi.

Rais Magufuli aisifia ‘Sizonje’ ya Mpoto, ategua fumbo la mashairi yake
Chid Benz: Huwezi Kunifananisha na Joh Makini