CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa kukiuka sheria na taratibu katika kushughulikia watuhumiwa wa biashara za dawa za kulevya nchini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freemana Mbowe, ambapo amesema majaji waliopangiwa katika kesi hiyo inayokusudiwa kusikilizwa Februari 21 ni pamoja na Jaji Sakiety Kihiyo, Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Khaday.
Amesema kuwa Chadema inakubaliana na inaunga mkono mapambano dhidi ya uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya lakini staili anayoitumia Makonda inawafanya watuhumiwa kuukimbia mkono wa sheria.
“Sisi Chadema tunakubaliana na kabisa na mapambano dhidi ya waingizaji na watumiaji wa dawa za kulevya nchini lakini kwa staili ambayo Makonda anaitumia ni kuwaandaa wafanyabiashara wanaotuhumiwa kuukimbia mkono wa sheria”amesema Mbowe
Aidha, akikabidhi ripoti hiyo yenye majina 92 ya watuhumiwa wa dawa za kulevya yakiwemo majina ya watoto wa viongozi kwenye uongozi wa Serikali ya Awamu ya Pili, Tatu na Nne, Makonda alisema kwamba yeye (Makonda) na Kamishna wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Simon Sirro, waliamua kutaja majina hadharani kwa kuwa biashara inafanyika hadharani.
Hata hivyo, Vita ya kupambana na uingizwaji na utumiaji wa dawa za kulevya ilitangazwa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaa, Paul Makonda (Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Dar es Salaam) huku wafanyabiashara, viongozi wa dini na wanasiasa wakitajwa kuwa ni miongoni mwa watuhumiwa.