Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kukutana mjini Dodoma kwa lengo la kufanya mijadala kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi nchini.
Chama hicho kimepanga kufanya mikutano yote ya Baraza Kuu, Sekretarieti na Mkutano wa Kamati Kuu mjini hapo mwishoni mwa mwezi huu ikiwa ni mara ya kwanza kwa chama hicho kikuu cha upinzani kukutana katika mji huo ambao ni ngome ya CCM na pia makao makuu ya nchi.
Kwa mujibu wa mkuu wa idara ya habari na mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene, mikutano hiyo itaanza Mei 28.
“Baada ya kikao cha Baraza Kuu, sekretarieti ya Chama Makao Makuu itaketi Mei 28 na kisha Kamati Kuu nayo itaketi Mei 29,” Makene anakaririwa na Mwananchi.
Makene alieleza kuwa wameamua kufanyia mkutano huo Dodoma ambayo ni Kanda ya Kati ya chama hicho inayojumuisha mikoa ya Singida na Morogoro ikiwa ni sehemu ya uamuzi wake wa kuzipa nafasi kanda kuandaa mikutano mikuu.
Kamati Kuu ya Chadema inaketi mjini Dodoma ikiwa ni miezi miwili tu baada ya Kamati Kuu ya CCM kukutana mjini humo ambapo ni makao makuu ya chama hicho tawala.