Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeilalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa madai kuwa inatengeneza mazingira ya kuiandalia CCM ushindi wa ‘bao la mkono’ kwa kutovipa vyama vya siasa nakala ya daftari la kudumu la wapiga kura kama ilivyofanya mwaka 2010.

Malalamiko hayo ya Chadema yametolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, John Mnyika alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Mnyika alieleza kuwa utaratibu wa vyama vya siasa kupewa dapewa nakala ya daftari la kudumu la wapiga kura huvisaidia vyama vya siasa kuwasaidia wananchi wao pale wanapokwama kupiga kura kutokana na mapungufu ambayo huwa yanajitokeza wakati wa upigaji kura, hususan pale wapiga kura wanapokuta majina yao hayako katika orodha ya majina yaliyopo vituoni.

“Daftari hili ni muhimu, mwaka 2010 tuliweka dawati letu kwenye vituo. Wananchi ambao walifika vituoni na kukosa majina yao kwenye orodha iliyobandikwa tuliwaambia waende kwenye daftari la Chadema waangaliziwe majina yao na waliokuta majina yao walipewa nafasi ya kupiga kura,” alisema Mnyika.

Kadhalika, Myika aliitaka NEC kuiruhusu timu ya mifumo ya Tehama ya Chadema pamoja na waangalizi wa Uchaguzi kukagua program itakayotumika kuhesabia kura za urais ili kujiridhisha na zoezi zima la kupokea na kuhesabu kujumlisha kura.

Kufuatia matamkohayo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva ameeleza kuwa Chadema ndicho chama pekee kinachoipa Tume shida kwa kuwa kimekuwa na wasiwasi mara kwa mara kuhusu masuala ya mbalimbali yanayofanywa na tume hiyo.

Jaji Lubuva ameeleza kuwa Tume imepanga kukutana na wawakilishi wa vyama vitavyoshiriki katika uchaguzi mkuu ili waweze kujadili dukuduku zao.

Hata hivyo, tume imekubali ombi la Chadema kuwaruhusu wataalam wa Tehama wa chama hicho pamoja na waangalizi wa uchaguzi kutembelea na kukagua program ya kujumlishia kura za urais.

Van Gaal Awasihi Wachezaji Wa Man Utd
‘Toroka Uje Ya Ukawa’ Kusomba Vigogo Hawa Wa CCM..?