Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kuwa jeshi la polisi linaendelea kumshikilia dereva wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe baada ya kumkamata nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, dereva huyo aliyetajwa kwa jina la Urassa amekataliwa kupewa dhamana na kwamba hakuna mtu yeyote aliyeruhusiwa kumuona.
Amesema kuwa kutokana na hatua hiyo, wanapata wasiwasi wa hali ya kiafya ya mfanyakazi wao kwani hata mwanasheria amezuiwa kumuona.
-
Uganda kuwatambua Wahindi kama kabila
-
Video: Katibu Tawala wilaya ya Kinondoni awafunda wahitimu wa ufundi Cherehani
“Tunalaani na kukemea vikali kitendo hicho cha jeshi la polisi ambacho ni mwenendo unaopaswa kuachwa mara moja, kwa jeshi hilo kujipatia mamlaka lisilokuwa nayo, hasa kuwakamata watu na kuwashikilia chini ya ulinzi kinyume cha sheria,” imeeleza taarifa ya Chadema.
Katika hatua nyingine, Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jana iliwafutia dhamana Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiku na kuamuru wawekwe rumande baada ya kudaiwa kukiuka masharti ya dhamana zao.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa hakuwa katika nafasi ya kuzungumzia ya Chadema, kwani alikuwa akihudhuria msiba wa askari wa jeshi la ulinzi waliouawa wakilinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.