Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro kimemvua Somon Mmari uenyekiti wa wilaya hiyo, baada ya kumtia hatiani kwa usaliti.
Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Utendaji ya chama hicho ngazi ya wilaya, ikieleza kuwa mbali na makosa ya usaliti, imemtia hatiani pia kwa makosa mengine matatu.
Imeelezwa kuwa Mmari amekuwa akitumia mikutano ya mbunge wa jimbo hilo, Dkt. Godwin Mollel (CCM) kuwashutumu baadhi ya madiwani wa chama hicho.
Akizungumzia uamuzi huo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema kuwa uamuzi huo umefikiwa jana mchana katika kikao husika.
“Hizo taarifa ni za kweli. Kikao kimemalizika mchana huu (jana) na kufikia uamuzi huo. Moja kati ya mambo yaliyomuondoa ni madai ya kukiongoza chama kwa migogoro isiyoisha,” Lema anakaririwa na Mwananchi.
Alipotafutwa kuzungumzia taarifa hizo, Mmari ambaye ni Diwani wa Kata ya Nasai alikataa kuzungumzia hilo akieleza kuwa hajapata taarifa rasmi na kwamba taratibu za chama hazimruhusu kuzungumzia hilo ikiwa bado ni mapema.
Mkoa wa Kilimanjaro ni kati ya ngome za Chadema zilizoathiriwa na hatua za madiwani wake pamoja na wabunge kukihama chama hicho na kutimkia CCM.