Mkutano Mkuu wa Chadema leo umebariki rasmi jina la Edward Lowassa kuwa mgombea urais wa chama hicho pamoja na aliyekuwa kada mkongwe wa CUF, Juma Haji Duni kuwa mgombea mwenza.

Kwa mujibu wa sheria, Juma Haji Duni amelazimika kukihama kwa muda chama chake cha CUF ili aweze kukidhi kigezo cha kuwa mgombea mwenza wa mgombea urais wa Chadema. Kwa pamoja watapeperusha bendera ya Ukawa.

Akizungumza katika mkutano mkuu huo baada ya kupiga kura ya wazi, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema kuwa uteuzi huo na utaratibu wote uliofanyika umezingatia katiba ya chama hicho kama ilivyokuwa katika awamu zilizopita.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimewakaribisha rasmi waliokuwa wanachama wa CCM wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa wenyeviti wote wa CCM taifa, Mgana Msindai.

Aidha, Mwenyekiti wa Chadema ametangaza rasmi kubadili kauli mbiu ya ‘Safari ya Matumaini’ iliyokuwa ikitumiwa na Lowassa, na sasa itakuwa ‘Safari ya Uhakika’.

“Safari ya Matumaini inaonekana kama ni safari ya mashakamashaka hivi, sasa hivi. Sasa tunaibadili itakuwa ‘Safari ya Uhakika,” alisema Mbowe.

 

Juventus Wamkaushia Oscer
Man Utd Wamalizana Na Lyon Ishu Ya Rafael