Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuwa kinaamini barua za kujiuzulu zilizosainiwa na waliokuwa madiwani wa wilaya ya Hai hazikuandikwa na madiwani hao bali ziliandikwa na mtu mmoja aliyewashawishi na wao kutia sahihi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Helga Mchomvu (Chadema) jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa baada ya kupokea na kusoma barua hizo alibaini hazikuandikwa na madiwani hao kwani zilikuwa zimekosewa Kata na majina ya wahusika kitu ambacho sio cha kawaida kwa diwani kusahau jina la eneo alilokuwa analiongoza.
“Ukiangalia barua iliyoandikwa Julai 25, aliyekuwa diwani wa kata ya Mnadani, Ernest Kimath inaonesha alikuwa diwani wa Weruweru na sio Mnadani. Lakini mwisho wa barua inaonesha jina la diwani huyo,” alisema Helga.
- Sakaya amshukia Maalim Seif, ahofia uwezo wake wa kufikiri
- Video: Majaliwa awaonya wapiga dili, asema cha moto watakiona
Aliongeza kuwa kwa namna hiyohiyo, barua iliyoonesha kuwa iliyoandikwa na aliyekuwa diwani wa Weruweru, Abdallah Chiwili ina maelezo yanayoonesha kuwa alikuwa diwani wa kata ya Mnadani.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa halmashauri ya Hai alisema kuwa pamoja na upungufu huo uliobanika amezipokea barua hizo na kuridhia uamuzi wa kujiuzulu kwao.
Kwa upande wake Chiwili ambaye ni miongoni mwa madiwani waliojiuzulu na kujiunga na CC alikiri kuwa barua zao zilikuwa na makosa hayo yaliyobainishwa. Alisema makosa hayo yalijitokeza kwakuwa aliyezichapa ni mtu mmoja.
Chiwili amesisitiza kuwa wao walifanya maamuzi bila kushinikizwa na mtu yeyote bali uamuzi wao ulitokana na kuridhishwa na utendaji wa Rais John Magufuli.