Ngome ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Songwe ambayo awali ilikuwa ndani ya Mbeya imepata pigo baada ya madiwani wake watatu kutangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Madiwani hao kutoka Tunduma ambao walipokelewa na mkuu wa wilaya ya Momba, Jumaa Irando ni Ayubu Mlimba wa Mwaka Kati, Simon Mbukwa wa Kaloleni na Amos Nzunda wa Mpemba.
Wakizungumzia sababu za uamuzi huo, wamesema Chadema wamekuwa hawazingatii demokrasia na kuendesha chama hicho kwa ubabe.
“Si unajua baraza la madiwani Tunduma linaendeshwa na Chadema. Sasa tunapewa maagizo ya nini cha kuzungumza na kusimamia hata kama hayaendani na mahitaji ya wananchi wetu kwa lengo tu la watu wachache ndani ya chama,” Nzunda anakaririwa.
- Conte: Kama wanadhani sifanyi vizuri wafanye maamuzi
- LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Februari 7, 2018
Waliongeza kuwa wameona wajiunge na CCM kwani wamebaini kuwa walichokuwa wanakipigania wakiwa katika chama hicho kikuu cha upinzani hivi sasa kinatekelezwa kikamilifu na Serikali.
Mbeya ni moja kati ya mikoa ambayo inaaminika kuwa ngomea ya Chadema lakini sasa imeanza kumegeka kwa madiwani wake kujiuzulu.
Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Tunduma, Boniface Mwakabanje amesema madai yao sio ya kweli na kwamba ataitisha kikao cha dharura cha madiwani wote wa chama hicho kujadili.