Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa inakihujumu kwa kutengeneza kadi za ziada zaidi ya milioni 2 ili kukipa ushindi Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Akiongea na waandishi wa habari, mgombea ubunge  jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Saed Kubenea ameeleza kuwa wamepata kadi 100 kati ya kadi hizo ambazo zimewasilishwa kwao na baadhi ya wafanyakazi wa NEC wanaowataja kama ‘Wasamalia Wema’ waliowapa taarifa ya kuwepo idadi hiyo kubwa ya kadi.

“Tunashukuru kuna wasamaria wema ndani ya NEC ambao hawakubaliani na hujuma hizo, wameamua kutuambia na wametuahidi kutupatia kadi nyingine zaidi,” alisema Kubenea.

Kubenea amesema kuwa amezikabidhi kadi hizo kwa mwanasheria ambaye amemuapisha kabla ya kuzipokea kwa ajili ya hatua zaidi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva amekanusha taarifa hizo na kudai kuwa kama Chadema wanaamini kuwa kadi hizo zimetayarishwa na tume hiyo, wangeziwasilisha kwao.

“Kama Chadema wamesema kadi hizo ni za kwetu ni vema wangezileta kwetu ili tuone kama kweli ni zenu, kwa kuwa wamezungumza hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari na mimi sijaziona kadi hizo siwezi kuzungumza,” Alisema Jaji Lubuva.

AC Milan Wadhamiria Kukilinda Kipaji Cha Balotelli
Juventus Kukamilisha Ya Juan Cuadrado Leo