Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema kimetoa tamko lake kufuatia tuhuma mbalimbali zilizotolewa na aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa.

Tamko hilo lililotolewa na mkuu wa Habari na mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene, limeeleza kuwa kwa sasa chama hicho hakitajiingiza katika mijadala hiyo bali kitajikita zaidi katika Kampeni zinazoendelea.

“Tumesikia alichosema Dk. Slaa, lakini nguvu yetu, akili zetu na miili yetu imejikita katika kampeni na kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu ndio kipaumbele chetu cha kwanza,” alisema Makene.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema kuwa Dk. Slaa alishiriki katika vikao vyote vya ngazi za juu vya chama na kwamba uamuzi uliofanyika ni uamuzi wa chama na sio uamuzi wa mtu mmoja.

Mbowe alifananisha kuondoka kwa Dk. Slaa wakati huu wa kampeni kama kuruka nje ya dirisha la treni ya Kigoma wakati safari ya chombo hicho inaendelea. Aliongeza kuwa ajenda kuu ya Umoja wa chama hicho hivi sasa ni kufanya mabadiliko nchini na sio vinginevyo.

“Hiki chama hakimilikiwi na mtu mmoja, hata mimi. Kama mtu yoyote na mke wake hawataki kulikomboa taifa, acha watupishe,” alisema.

 

Rostam Aibuka Na Kumjibu Dk Slaa
Enyeama Aigwaya Taifa Stars