Wanawake wanne wamefariki na wengine 13 wamejeruhiwa baada ya muuzaji kumwaga chai kwenye moto na hivyo kusababisha taharuki kwenye Uwanja wa Green wa Kericho, wakati wa sherehe za Mashujaa Day mwaka huu.
Taarifa ya Polisi Nchini Kenya, imesema tukio hilo la kusikitisha lilitokea masaa kadhaa kabla ya milango ya uwanja kufunguliwa kwa umma kwa ajili ya sherehe za kitaifa zilizongozwa na Rais William Ruto.
“Vurugu zilisababishwa na mwanamke aliyekuwa akiuza chai nje ya uwanja ambaye kwa bahati mbaya alimwaga chai moto karibu na “Lango C” kando ya barabara ya umma, kufuatia hilo, umma ulipatwa na taharuki na kufikiri ni gesi ya machozi imerushwa kwao,” ilisema Polisi.
Waliojeruhiwa, ambao wanasemekana kuwa katika hali thabiti, walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kericho wakati waliokufa walipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali huku wakisubiri kutambuliwa na kufanyiwa upasuaji wa kufafanua chanzo cha kifo.