Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluh Hassan kuvifungulia Vyuo vilivyopo chini ya Taasisi za dini, vilivyofungwa miaka miwili iliyopita.

Chalamila ameyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio na miradi iliyotekelezwa ndani ya miaka miwili, hii leo Machi 16, 2023 katika viwanja vya mashujaa (Mayunga), vilivyopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila akipokea tuzo ya heshima kwa niaba ya Rais Dkt. Samia katika hafla ya kumpongeza katika utawala wake w ndani ya miaka miwili.

Amesema “tuna maombi yetu ya vile vyuo ambavyo vilifungwa, vyuo hivi vinavyomilikiwa na Kanisa la Katoliki na KKKT hapa kwetu tunaomba navyo Rais ungeangalia wazo la angalau kuvifungua, ili Mkoa wetu uweze kuwa vizuri na mambo yaendelee.”‘

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila amesema mpaka sasa miradi mbalimbalu imetekelezwa vyema na inaendelea kutekelezwa ikiwemo miradi ya maji, barabara, umeme, afya na elimu.

“Serikali ya awamu ya sita imefanya mambo makubwa sita ikiwemo upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi mijini na vijijini lakini pia utatuzi wa changamoto za uchumi na kijamii unaowakabili wananchi,” amesema Nguvila.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa ya Chama cha Mapinduzi – CCM, Mkoa wa Kagera, Karim Hamza ametoa wito kwa madiwani pamoja na Viongozi kuanzia ngazi ya kata, kuendelea kutatua changamoto za wananchi bila kubagua ili kutekeleza vyema ilani ya chama.

Wiki ya Maji: Majaliwa asisitiza uhifadhi wa Mazingira
Walimu wathaminiwe, walindiwe utu wao: Kairuki