Kwa mara ya kwanza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila atakuwa shuhuda wa Masumbwi tangu alipoteuliwa kuwa kiongozi wa Mkoa huo, akichukuwa nafasi ya Amos Makalla aliyehamishiwa mkoani Mwanza.
Chalamila aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera anatarajiwa kujumuika na Mashabiki wa mchezo wa Masumbwi katika pambano la Kimataifa litakalorindima mwishoni mwa juma lijalo kati ya Bondia wa Tanzania Selemani Kidunda dhidi ya Erick Mukadi wa DR Congo.
Pambano hilo lisilo la ubingwa uzito wa kati raundi 10, litafanyika Jumamosi (Juni 30), katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam.
Promota wa pambano hilo, Fadhili Maogola amesema maandalizi ya pambano hilo yanaendelea vizuri, na wamefurahishwa kufuatia ombi lao la kumualika Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila kuwa mgeni rasmi kukubaliwa.
Amesema kiongozi huyo atajumuika na mashabiki wa mchezo wa masumbwi kushuhudia mapambano nane ambayo yatarindima siku hiyo.
“Siku ya pambano tunatarajiwa kuwa na mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila pamoja na Naibu wa Waziri wa UtamadunĂ, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA”, ” amesema Maogola.
Promota huyo amesema pamoja Kidunda kucheza siku hiyo, lakini mabondia Mfaume Mfaume na Plus Mpenda watapambana na mabondia kutoka nje ya nchi.
“Mfaume atacheza na Nkululeko Mhlongo wa Afrika Kusini wakati Pius Mpenda atapigana na Simon Tcheta wa Malawi,” amesema Maogola.