Katika hali ya ‘KUSTAAJABISHA’ uongozi wa klabu ya Simba SC bado haujamalizana na kiungo mshambuliaji kutoka nchini Zambia Clatous Chama, licha ya kaimu mwenyekiti wa klabu hiyo Mwina Kaduguda kutamba mbele ya waandishi wa habari.

Mwanzoni mwa mwezi huu Kaduguda alitamba kwenye mkutano na waandishi wa habari kuwa, uongozi wa Simba SC chini ya Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Mohamed Dewji ‘Mo’ umekamilisha mpango wa kumbakisha kiungo huyo hadi mwaka 2023, kwa kiasi cha shilingi milioni 700.

Taarifa zilizoibuka hii leo Jumatatu (Desemba 28) zinaeleza kuwa, Chama, kwa sasa yupo kwenye mazungumzo na mabosi wa Simba SC akishawishiwa kuongeza mkataba mpya ndani ya klabu hiyo.

Habari kutoka ndani ya Simba SC zimeeleza kuwa, pande hizo mbili zimefikia hatua nzuri ya mazungumzo, jambo linalotoa matumaini kwa Chama kusaini mkataba mpya.

“Kwa sasa bado Chama hajasaini mkataba na amekuwa kwenye mazungumzo na viongozi ili aweze kusaini kwani ni mchezaji muhimu ndani ya kikosi.”

“Imekuwa akitajwa kuwa kwenye mazungumzo na Young Africans jambo linalowapa presha viongozi hasa ukizingatia ni mchezaji muhimu kikosi cha kwanza,” ilieleza taarifa hiyo.

Mkataba wa Chama ndani ya Simba SC kwa sasa umebakiza miezi sita na anaruhusiwa kuzungumza na timu ambayo inahitaji huduma yake kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka duniani (FIFA).

Ndani ya Simba SC kwa msimu wa 2020/21, Chama amehusika kwenye mabao 12 kati ya 33 ambapo amefunga mabao sita na kutoa pasi sita za mabao.

Mauricio Pochettino adaiwa kutua PSG
Rais Magufuli amtumbua Mkurugenzi Igunga

Comments

comments