Kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama amewaomba radhi mashabiki na wanachama wa klabu hiyo baada ya kukosa mataji katika msimu huu huku akiwaambia kuwa mengi yanakuja msimu ujao 2023/24.

Simba SC ilianza kwa kupoteza mwelekeo baada ya kutolewa katika Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kisha ikabanwa na Namungo FC kwa sare ya 1-1 matokeo ambayo yaliipa nafasi Young Africans kuusogelea Ubingwa wa Tanzania Bara na siku kadhaa zilizofuata iliondolewa kwenye Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ kwa kufungwa 2-1 na Azam FC katika mchezo wa Nusu Fainali kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Chama amesema kuwa wao wachezaji wamechukizwa kukosa kombe lolote katika msimu huu huku wakijipanga vizuri kuhakikisha wanabeba mataji yote ya ndani katika msimu ujao.

Kiungo huyo kutoka nchini Zambia amesema kitu kingine walichokipanga ambacho lazima wakitimize ni kufuzu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika msimu ujao, baada ya kuishia Robo Fainali katika misimu minne tofauti.

Ameongeza kuwa zipo sababu nyingi zilizosababisha wao wapoteze yote katika msimu huu, lakini uzuri kwamba viongozi na benchi la ufundi lililo chini ya Mbrazili, Robert Oliviera ‘Robertinho’ wanafahamu walipokosea hivyo watarejea kivingine msimu ujao.

“Zipo sababu nyingi zinazoweza kupelekea kukosa ubingwa timu yoyote ikakosa ubingwa kama ilivyokuwa kwetu, wakati mwingine sababu zinaweza kuwa nje au ndani ya uwanja.

“Tuwaambie mashabiki na wanachama wa Simba kuwa tutarejea msimu mwingine na zaidi kupambania ubingwa wa ligi na Kombe la ASFC, tunafahamu tulipokosea tutarejea tukiwa kamili kufanikisha malengo yetu.

“Hakuna kitakachoshindikana kwetu, zaidi ya sisi wachezaji wenyewe kufahamu sababu iliyosababisha kukosa makombe msimu huu,” amesema Chama

Fahamu Kuhusu Zombie Apocalypse ya Meridianbet
Azizi Ki: Msimu ujao nitakiwasha zaidi