Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama, ameeleza kufurahishwa kwake kuanza Iigi kwa kufunga mabao kwenye viwanja vya mikoani kitu ambacho misimu ya nyuma kilikuwa kigumu mno kwake, akitabiri anaweza kuwa na mabao mengi zaidi msimu huu kuliko wakati mwingine wowote tangu acheze soka nchini.
Kiungo huyo kutoka nchini Zambia amesema wakati timu yake ya Simba SC ikipata ushindi mara tatu mfululizo kwenye viwanja vya ugenini, na yeye ameshafunga mabao mawili kitu ambacho hajawahi kukifanya tangu atue nchini.
“Kusema ukweli nimefurahi sana, kwa misimu mingine tangu nicheze soka hapa Tanzania nimekuwa nikipata shida sana kufunga mabao kwenye hivi viwanja vya mikoani kwani kuna wakati vinakuwa havipo katika hali nzuri, lakini mpaka hii raundi ya tano nimefunga mabao mawili ugenini,” amesema.
Chama alifunga bao la kwanza, Agosti 17 kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Simba SC ikiichapa Mtibwa Sugar mabao 4-2 na Alhamisi iliyopita alipachika bao la pili msimu huu kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, akiiongoza timu yake kushinda 3-1 dhidi ya Prisons. Mabao yote hayo aliwafunga kwa kutumia mguu Wa kushoto.
Chama amesema kama ameanza kufunga kwenye viwanja vya mikoani ambavyo vilikuwa vigumu kwake, anaweza kufunga mabao mengi msimu huu pale Uwanja wa Benjamin Mkapa utakapofunguliwa.
Amesema amekuwa akifunga mabao kadhaa kwenye Uwanja huo na ana uhakika atafanya hivyo msimu huu, na akiongeza na mabao ambayo kwa sasa anafunga mikoani anaweza kuwa na idadi kubwa ya mabao msimu huu kuliko wakati mwingine wowote.
“Najua Uwanja wa Benjamin Mkapa utafunguliwa muda si mrefu kwa hiyo ni hali nzuri kwangu, naomba Mungu anisaidie na wachezaji wenzangu pia wanipe msaada, naweza kuwa kwenye kinyanganyiro cha ufungaji bora msimu huu,” amesema