Kiungo kutoka nchini Zambia na klabu ya Simba SC Clatous Chama amewapongeza wachezaji wenzake kwa kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya RS Berkane katika mchezo wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika, uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa jana Jumapili (Machi 13).
Kanuni zimemzuia Chama kushiriki michuano hiyo akiwa na kikosi cha Simba SC, kwani usajili wake kimataifa unasomeka yupo RS Berkane na alicheza hatua za awali.
Chama amesema kwa Simba SC utamaduni kuhakikisha wanashinda kila mchezo wanaocheza Uwanja wa Benjamin Mkapa, wachezaji wamefanikisha hilo.
“Sisi ni kawaida yetu, tunapocheza Uwanja wa Mkapa tunajiwekea malengo ya kushinda, nawapongeza wachezaji wenzangu kwa ushindi huu muhimu.”
“Sasa tumefikisha alama saba, tunaongoza kundi D, tuna nafasi nzuri ya kuingia robo fainali. Tunajipanga vizuri kuhakikisha tunakamilisha malengo yetu katika michezo miwili iliyobakia,” amesema Chama
Simba itasafiri hadi nchini Benin kuikabili ASEC Mimosas March 20 na baadae kurejea jijini Dar es salaam kukamilisha mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya USGN April 03.