Viungo Clatous Chama na Fabrice Ngoma wakitarajiwa kuwasili nchini Uturuki kwa ajili ya msimu wa 2023/24, huku wakiandaliwa Programu maalum za mazoezi kabla ya kuungana rasmi na wenzao.
Chama na Ngoma wanatarajiwa kuwasili Uturuki wakati wowote, mara baada ya kumalizika kwa taratibu zao za kuomba vibali vya kusafiria ambapo watakuwa ndio nyota wa mwisho kati ya wale ambao walikuwa wametambulishwa kuwasili kambini.
Juzi Jumanne (Julai 18), Simba SC iliwapokea mastaa wao wanne ambao ni Che Malone Fondoh, Jean Baleke, Aubin Kramo Kouame na Willy Onana ambao walisalia jijini Dar es Salaam.
Mara baada ya kuwasili Chama na Ngoma, nyota hao wanatarajiwa kuanza na mazoezi ya kuongeza utimamu wa mwili ‘gym’, kabla ya kufanyishwa mazoezi ya kukimbia mbio ndefu na baada ya hapo ndiyo wataungana na program za pamoja na wenzao.
Meneja wa Simba SC, Mikael Igendia, amesema: “Tumewapokea wachezaji wanne ambao rasmi walianza program za mazoezi siku ya Jumatano, lakini tunafahamu kuwa bado kuna mastaa wengine ambao wanaendelea kuja.
“Kama ilivyokuwa kwa Che Malone, Kramo, Onana na Baleke watakaowasili wataanza na program mbili za utimamu wa mwili kabla ya kuungana na wenzao kwenye mazoezi ya pamoja.”