Kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chama amewataka Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kukaa mkao wa kula kupata Burudani kutoka kwenye kikosi chao, huku akiahidi msimu huu watafanya vizuri na watapambana kuhakikisha wanatimiza malengo.
Chama ambaye ni sehemu ya wachezaji waliowasili jijini Tanga jana Jumanne (Agosti 08) majira ya usiku tayari kwa mchezo wa Nusu Fainali wa Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Fountain Gate, amesema wamejiandaa vizuri, hivyo ni deni kwao kuhakikisha wanawapa Mashabiki na Wanachama furaha inayostahili.
Hata hivyo Kiungo huyo amesema anatambua ushindani utakuwa mkubwa kutokana na timu zote kuwa katika maandalizi kabambe ya kuelekea msimu ujao, lakini amesisitiza Simba SC inahitaji kitu baada ya kutoka kapa kwa msimu miwili mfululizo.
“Ushindani utakuwa mkubwa kwa kuwa kila timu inahitaji kupata matokeo na imesajili vizuri kukabiliana na ushindani. Nafikiri mashabiki wakae wakisubiri kuona tutawapa nini msimu huu kwa kuwa tumepania sana kuonyesha kiwango cha juu na naamini kuwa tutakuwa na timu bora.” amesema Chama na kuongeza kuwa msimu uliopita hawakuweza kupata mataji jambo linawafanya kutambua wana deni kubwa kwa wanasimba wote.
Simba SC itaanza kampeni ya kuwania Ngao ya Jamii 2023 kesho Alhamis (Agosti 10) kwa kucheza dhidi ya Singida Fountain Gate majira ya saa moja usiku, katika Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Mshindi wa mchezo huo atacheza Fainali na mshindi wa mchezo wa leo Jumatano (Agosti 09) kati ya Mabingwa watetezi Young Africans dhidi ya Azam FC.