Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Olivieira ‘Robertinho’ amewapa kazi maalum viungo washambuliaji wawili wa timu hiyo, Clatous Chama na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ kuhakikisha wanamtengenezea mshambuliaji, Jean Baleke nafasi za kufunga.
Simba kesho Jumapili (April 16) wanatarajiwa kuikaribisha Young Africans katika mchezo wa Dabi ya Kariakoo ya mzunguko wa pili itakayopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Timu hizo zitaingia katika mchezo huu zikiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza ambao ulipigwa Oktoba 23, mwaka jana 2022, uwanjani hapo.
Robertinho amesema: “Tunaendelea na maandalizi ya mchezo huu, tunafahamu ubora wa Young Africans na mapungufu yao.
Licha ya ugumu wa mchezo lakini malengo yetu makubwa ni kuhakikisha tunashinda mchezo huu kwa kuwa tunaamini ni lazima kuonyesha ukubwa wetu.
“Tuna wachezaji bora na ambao wamekuwa kwenye kiwango bora katika mchezo michache iliyopita akiwemo Baleke na ni wazi tunataka kutumia faida ya ubora wake na ubunifu wa viungo kama Chama na Saido kutengeneza nafasi za kufunga.” amesema Kocha Robertinho
Hadi sasa Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 68, huku Simba SC ikiwa nafasi ya pili kwa kufikisha alama 60. Timu zote zimeshashuka dimbani mara 25 msimu huu 2022/23.