Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheikh Hasina ameshinda kwa kishindo uchaguzi mkuu na kumpa nafasi ya kuongoza kwa muhula wa tatu, huku chama chake kikizoa viti vya ubunge.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Tume ya Uchaguzi, chama tawala kimeweza kushinda viti 288 vya ubunge kati ya viti 300, ushindi ambao unazidi kishindo cha uchaguzi mkuu uliopita.
Hata hivyo, wapinzani wake wamelalamikia mchakato wote wa upigaji kura wakidai kuwa uligubikwa na vitisho, vurugu na uchakachuaji wa matokeo katika wilaya nyingi.
“Tunaitaka tume ya uchaguzi kutokubali kutangaza matokeo haya yaliyochakachuliwa mara moja. Tunataka uchaguzi mwingine uitishwe mara moja chini ya Serikali ambayo haina upande kwenye uchaguzi,” alisema kiongozi wa upinzani, Kamal Hossain.
Bunge la Bangladesh lina viti 350, kati ya hivyo wabunge 300 ni wakuchaguliwa na wanachi, viti 50 ni kwa ajili ya wabunge wanawake pamoja na wabunge wa viti maalum ambao wanatokana idadi ya kura za vyama husika.