Mwanamuziki nguli kutoka Uganda, Jose Chameleone amefunguka ya moyoni kuhusu uamuzi wa Harmonize kumuondoa kwenye wimbo wa ‘Inabana’ na kumuweka Eddy Kenzo, akieleza kuwa huenda hakupenda alichoimba.

Akifunguka katika mahojiano maalum aliyofanya jana na mtangazaji mmoja nchini Uganda, mkongwe huyo alieleza jinsi walivyokutana na Harmonize katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya na kupanga kufanya kazi.

Amesema mkali huyo wa ‘Kwangwaru’ alimuomba kumshirikisha kwenye wimbo wake na yeye alikubali kwakuwa anapenda anavyoimba.

Ameeleza kuwa walibadilishana namba za simu na anuani za barua pepe kwakuwa walikuwa na haraka. Baada ya muda mfupi alitumiwa beat (mdundo) akarekodi sehemu yake na kuwasilisha kwa Harmonize.

Kwa mujibu wa mkali huyo wa ‘Tubonge’, kupishana kulianza baada ya kuwa anapigiwa simu na meneja wa Harmonize akipewa maelekezo kwa ajili ya kufanya video, lakini yeye aliendelea kusisitiza kuwa angependa kuwasiliana na mwanamuziki mwenzake moja kwa moja. Kwa bahati mbaya haikuwa hivyo.

“Ndiyo, Harmonize ni msanii mkali sana lakini hata mimi sio mwanamuziki wa bei chee na ni msanii mkali pia. Lakini pindi nilipoomba nizungumze na Harmonize nadhani alikuwa bize sana na tulikuwa tumeshamaliza kurekodi wimbo na kilichokuwa kimebaki ni kufanya video tu,” alisema Chameleone kwa lugha ya Kiganda na kutafsiriwa Kiingereza na ripota wa SnS aliyeko Kampala.

“Kwahiyo, nilijiondoa mwenyewe kutoka kwenye mradi huu. Sitaki vitu vya kuhangaika sana na sipendi kukosewa heshima. Kwa miaka yote hii nimefanya muziki na sina nilichobakiza kuonesha kuwa naweza. Hivyo, nikawaambia kama yote yakimalizika basi tutaendelea, lakini mimi sina tatizo kwakuwa wanaopiga kasia kwenye mtumbwi, mmoja akiwa mbele na mmoja nyuma wote wanaelekea sehemu moja,” aliongeza.

Hata hivyo, Chameleone alimtetea Eddy Kenzo kwa kushiriki kwenye wimbo huo akiwataka mashabiki wasimlaumu kwani yeye alifanya kazi yake na mwenye uamuzi juu ya wimbo huo ni Harmonize mwenyewe.

“Inawezekana alipenda Eddy Kenzo alivyoimba na labda hakupenda mimi nilivyoimba lakini yote kwa yote yeye ndiye mwenye uamuzi, hata akisema amshirikishe Justin Bieber ni uamuzi wake,” Chameleone anakaririwa.

Sokomoko lilizuka mtandaoni baada ya video ya ‘Inabana’ ya Harmonize kutoka rasmi akiwa ameshirikishwa Eddy Kenzo, wakati sehemu ya wimbo huo aliyoshirikishwa Chameleone iliyokuwa imevuja mtandaoni awali haisikiki tena.

Baada ya kushambuliwa kila kona na mashabiki mtandaoni, Eddy Kenzo aliamua kujitetea hadharani akieleza kuwa yeye pia alipata mshtuko baada ya wimbo huo kuachiwa, aliposikia kuwa Chameleone alikuwa ameshirikishwa awali.

Amesema aliamua kumuuliza Harmonize na alikiri kuwa awali alirekodi na Chameleone lakini kulitokea kutoelewana akaamua kubadili uamuzi.

Kenzo amesema hana hatia katika hilo kwani alifanya kazi bila kujua kilichokuwa kimefanyika awali na hakuwa na lengo la kumkosea heshima Chameleone.

Mdogo wake Chameleone, Weasel alikuwa mmoja kati ya wanamuziki wa Uganda waliomvaa Eddy Kenzo wakidai amemkosea heshima mkongwe huyo.

Miili ya ajali ya Lori la Dangote yashindwa kutambulika
Wafanyabiashara 300 kutoka Uganda kutua Tanzania