Serikali nchini imesisitiza uwepo wa haja ya kuwa na tafiti nyingi za afya ambazo zitasaidia kutambua changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Mkurugenzi wa Huduma za Afya na Ustawi wa Jamii kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ntuli Kapologwe ameyasema katika mkutano unaoendelea wa tathmini ya miradi ya afya.

Amesema kuna umuhimu wa kupata tafiti nyingi ambazo zitaisaidia kuimarisha sekta ya afya nchini hali itakayomaliza matatizo mbalimbali kwa wakati muafaka.

“Kuna haja ya tafiti hizo ziunganishe sera na utekelezaji na zisiishie tu kwenye machapisho, ila zifike kwa wahusika na kutekelezwa kama ambavyo tafiti zinaelekeza” Amesema Kapologwe.

Mkurugenzi huyo ambaye alikua akiongea kwa niaba ya mgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo, ameongeza kuwa suala la tafiti za namna hiyo haziwezi kuepukika.

Ameongeza kuwa  kipimo cha utendaji kazi kwa sasa kipo kwa mwananchi kwa kuhakikisha wanapata mahitaji yote ambayo ni muhimu, na hasa masuala ya Afya.

“Na ipo haja kwa Vyuo nchini kushirikiana na Ofisi za Mkuu wa Mkoa na Wilaya, kwani kwa kipindi kifupi matatizo mengi yataweza kugundulika kwa haraka.” Amefafanua Kapologwe.

Mkutano huo ambao umeandaliwa na Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Mkoani Morogoro, unafanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa Morena Hotel, na unatarajia kumalizika Septemba 25 mwaka huu.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 25, 2019
Vijana washauriwa kuacha dhana ya kuajiriwa