Tanzania imepokea shehena ya Chanjo ya Janssen Dozi 115,200 kutoka Serikali ya Ubeligiji kupitia mpango wa COVAX Facility utaosaidia kuchanja wananchi 115,200 ili kuwakinga dhidi ya UVIKO-19.
Akizingumza na waandishi wa habari katika uwanja wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam baada ya kupokea Chanjo kutoka kwa Balozi wa Ubeligiji nchini Tanzania Peter Van Acker Dkt. Gwajima amesema kuwa, Serikali itaendelea kutoa chanjo dhidi ya UVIKO-19 katika vituo mbalimbali vya Afya ili kuwakinga Wananchi.
Amesema kuwa, awamu ya kwanza Serikali ilipokea dozi 1,058,400, awamu ya pili dozi 169,000 na leo Desemba 3, 2021 hivyo kufanya jumla ya Chanjo aina ya Janssen zilizopokelewa hapa nchini kufikia Dozi 1,342,600 na kufanya jumla ya chanjo zote zilizopokelewa kuwa dozi 4,421,540 zikiwemo chanjo ya Sinopharm na Pfizer ambazo zitachanja watu 2,882,545 .
Aidha Dkt Gwajima amewaagiza viongozi na watendaji wa ngazi zote kutoa ushirikiano wa hali ya juu kuhamasisha jamii kujitokeza kupata chanjo na kisha kujikinga kwa kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko 19 ikiwa ni pamoja na uvaaji wa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono (Sanitizer), kufanya mazoezi na kuepuka misongamano isiyo yalazima.