Jeshi la Zima Moto na Uokoaji limetoa elimu kwa wananchi kuhusu vyanzo vya magari kuwaka moto yawapo safarini na jinsi ya kujieupusha na majanga hayo.
Akizungumza katika kipindi cha On The Bench kilichoandaliwa na Dar24 Media, ambacho hufanyika mtaani kwa kuwakutanisha wataalam, viongozi na wananchi wa kawaida, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, Elnimo Shang’a alisema kuwa chanzo kikuu cha moto kwenye magari ni mifumo ya moto kutohakikiwa kabla na wakati wa safari.
Aliitaja mifumo hiyo kuwa ni pamoja na injini, betri na mfumo unaotoa mafuta kwenye tenki la gari kwenda kwenye injini ya gari. Hivyo, aliwasihi kuhakikisha kuwa pamoja na kuwa makini kuhakikisha mifumo hiyo haina tatizo na haiingiliwi wanapaswa pia kuhakikisha wana vizimia moto (fire extinguishers) vilivyokaguliwa, vinavyotunzwa kwa umakini pamoja na kuwa na elimu ya kuvitumia kwa ufasaha.
“Hivi vizimia moto ambavyo huwa viko kwenye magari vinatakiwa kufanyiwa ‘service’angalau mara moja kila mwaka. Lakini mara nyingi sisi huwa tunafanya ukaguzi, lakini mara nyingi hawa wanaovibeba wanavibeba kwa ajili ya kukwepa faini ya polisi wa usalama barabarani na sio kwa sababu ya usalama wa chombo chake,”alisema Shang’a.
Afisa huyo wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji aliongeza kuwa kwa sasa Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani kimeshirikiana na Jeshi la zima moto, hivyo hata askari wa usalama barabarani wanaweza kufanya ukaguzi wa kizimia moto kama kina ubora na kinaweza kufanya kazi ipasavyo.
Aidha, alitumia kipindi hicho kuwaelimisha madereva waliokuwa wamekusanyika pamoja na wananchi wengine kuhusu vizimia moto ikiwa ni pamoja na aina zake na jinsi vinavyotumika.
Katika hatua nyingi, Bruno Ndege ambaye ni mwalimu na mmiliki wa chuo cha ufundi wa magari cha Bruno VTC Buguruni Malapa, aliyekuwa katika kipindi hicho, alitoa ufafanuzi wa vyanzo vya moto kwenye magari yawapo safarini.
Akizungumzia magari makubwa hasa yanayosafirisha mafuta, ambayo yameripotiwa mara nyingi kuteketea kwa moto alisema yamekuwa katika hatari zaidi kwani yanatumia betri mbili zenye uwezo mkubwa wa moto. Hivyo, kwakuwa chanzo kikuu cha moto kwenye magari ni betri, zisipowekwa katika hali ya usalama zaidi kwenye magari hayo inakuwa hatari zaidi.
Aidha, alitoa somo jinsi ya kuweza kuepuka kuzuka kwa moto kwenye magari yawapo safarini.
“Hakikisha kitu cha kwanza unakagua, terminal betri zile ziko sawasawa? Je, zile terminal zimefungwa vizuri na spana? Na ukishazikagua ukazikuta ziko sawa unafungua gari lako kwenye boneti au kwenye kibini unaangalia zile nyaya ambazo ambazo zimefungwa kwenye starter motor, kuna nyaya zingine zimefungwa kwenye alternator kusiwepo na viungio vilivyolegea,” alisema mwalimu Ndege.
“Kwa sababu ajali ya moto sio mpaka tenki lianguke. Kuna magari mengine yanawaka moto yakiwa yanatembea kama hivi unasikia gari limewaka moto. Hizo husababishwa na betri, mfumo wa nyaya na chaji vinapokuwa vimelegea. Kwahiyo, dereva unapokuwa makini kukagua vile vitu utakuwa umevidhibiti
“Unapowasha gari, injini inapoanza kufanya kazi moja kwa moja alternator inaanza kuzalisha umeme. Na alternator haiwezi ikapata umeme bila betri. Sasa betri ikishapata umeme ukaingia kwenye alternator ili ianze kuzichaji betri. Ikiwa kuna ‘loose connection’ kwenye betri na zikawa zinatoka cheche kuna mawasiliano kama kuna tenki lenye leakage ndogo tu, cheche zile zinaweza kusababisha tenki likaripuka kama lina mafuta hata bila gari kuanguka,”aliongeza.
Mwalimu Ndege na Afisa wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji waliwasihi madereva na watu wanaomiliki magari kuepuka kununua vipuri visivyo na ubora kwani vinahatarisha usalama wa gari na vinaweza kuwa chanzo cha gari kuwaka moto.
Waliwataka watumiaji wa magari kutokubaliana na kinachodaiwa mitaani kuwa gari linaposafiri sana wakati wa jua hupata joto na huweza kusababisha kushika moto kuliko linapoendeshwa usiku.
Nao baadhi ya madereva walieleza kuwa baadhi ya wamiliki wa magari wamekuwa wakinunua vipuri kwa kuangalia unafuu wa bei badala ya kuangalia ubora, hali inayowaweka katika hatari ya kupata matatizo yakiwemo majanga ya moto.