Ihefu FC imeendeleza Rekodi yake ya kuitesa Young Africans baada ya juzi Jumatano (Oktoba 04) kuilaza mabao 2-1 huku Mshambuliaji wa timu hiyo, Charles Ilanfya akieleza namna alivyomsoma Kipa Djigui Diara kabla ya kufunga bao la pili lililoipa ushindi.
Kipigo hicho kinakuwa cha pili katika msimu wa pili mfululizo baada ya msimu uliopita kupoteza kwa kichapo kama hicho na kutibua rekodi waliyokuwa nayo ya kucheza zaidi ya mechi 50 bila kupoteza.
Kabla ya mchezo huo Young Africans ilikuwa imecheza mechi saba mfululizo za msimu huu kwenye mashindano yake yote wakiwa hawajapoteza na kuwa kipigo cha kwanza kwao chini ya kocha mkuu, Miguel Angel Gamond.
Katika mechi hizo saba zikiwamo za kimataifa, Young Africans ilikuwa imeruhusu bao moja ikifunga 20 japokuwa timu hiyo haikuwa na mwanzo mzuri wa msimu walipopokonywa Ngao ya Jamii kwa Penati 31 dhidi ya Simba SC baada ya dakika 90 kuisha kwa suluhu.
Ilanfya amesema katika mchezo huo walijipanga kushinda kutokana na kile walichoelekezwa na Benchi la Ufundi kukifanyia kazi.
Amesema alitumia akili na umakini kumsoma Diara kabla ya kufumua shuti pembeni akieleza kuwa bado kazi inaendelea kuhakikisha hata mechi zinazofuata wanaendelea kushinda ili kujiweka pazuri.
“Mpira ni akili, licha ya kutangulia kutufunga hatukukata tamaa, tukafuata maelekezo na nilivyopata nafasi nikamsoma kipa alivyosimama nikaachia shuti hadi wavuni.
“Hakuna siri ya mafanikio zaidi ya kujituma, bado ni mapema na ligi ndio kama inaanza, kimsingi ni kuendelea kupambana kuhakikisha tunashinda kila mechi iliyo mbele yetu,” amesema Ilanfya.
Matokeo hayo yaliifanya Young Africans kushuka nafasi ya pili kwa Pointi tisa, huku lhefu ikichumpa hadi nafasi ya saba kwa Point sita baada ya timu zote kucheza mechi nne.