Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Mawasiliano), Dkt.Zainabu Chaula amezindua minara miwili ya mawasiliano iliyopo kwenye vijiiji vya Nyabilezi na Igando, vilivyopo wilayani Chato mkoani Geita, ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za mawasiliano.

Dkt. Chaula, amesema kuwa ujenzi wa minara hiyo umefanyika kwenye vijiji hivyo baada ya wananchi kuomba huduma za mawasiliano na serikali kujiridhisha kuwa mawasiliano hayapo kwenye maeneo hayo.

Amesema kuwa serikali imeamua kujenga minara hiyo kwa kutumia ruzuku ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambapo ujenzi wake umegharimu zaidi ya shilingi milioni 500.

Katibu Tawala wa mkoa wa Geita, Denis Bandesi amesema kuwa miundombinu ya mawasiliano ambayo imewekwa kwenye maeneo hayo itawasaidia wananchi kufanya mawasiliano na kuendesha biashara zao ili kuhakikisha kuwa uchumi wa kati unamgusa  mwananchi pale alipo.

Kwa mujibu wa mtendaji mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba mpaka sasa UCSAF ina miradi ya ujenzi wa minara ya mawasiliano sehemu mbalimbali nchini kwenye kata 998 ambapo hadi sasa ujenzi umekamilika kwenye kata 903, na zaidi ya wananchi milioni tano wanapata huduma za mawasiliano.

Menina : "Siwezi kutaja Dau langu"
Vandenbroeck: Yanga imefanya usajili mzuri