Kocha wa Simba, Roberto Oliveira Robertinho’ ametamba kuwa uzoefu na ubora wa beki wake wa kati, Che Fondoh Malone utakuwa silaha muhimu kwa safu ya ulinzi katika mchezo wa ufunguzi wa mashindano ya African Football League (AFL) dhidi ya Al Ahly, Oktoba 20 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Malone aliyesajiliwa na Simba SC akitokea Coton Sports ya Cameroon, amecheza mechi zote tisa za Simba SC katika mashindano tofauti msimu huu ambazo timu hiyo imeruhusu mabao saba huku ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja, ikishinda saba na kutoka sare mbili.
Robertinho amesema uwepo wa Malone una maana kubwa kwa safu ya ulinzi katika mechi dhidi ya Al Ahly ambayo wanajipanga kuhakikisha wanapata ushindi wa kishindo ili wajiweke katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya kwanza.
“Che Malone ni beki bora lakini amewahi kucheza na Al Ahly, hivyo asilimia za kushinda na kuweka heshima katika mchezo huo muhimu ni kubwa akiungana na Shomari Kapombe, Luis Miqusone, Mohammed Hussein na wengine.
“Safu ya ulinzi ni eneo ambalo kama halitakuwa sawa kuna uwezekano wa mchezo kuharibika ndio maana nguvu kubwa kwa sasa nimewekeza huko ili kumfanya mpinzani ashindwe kutumaliza,” amesema kocha Robertinho.
Kocha huyo amesema tofauti na mechi nyingi ambazo wameonekana kufanya makosa katika safu ya ulinzi ambayo yamewapa faida wapinzani wao, anaamini mechi dhidi ya Ahly itaonyesha uimara mkubwa katika ukuta wake kutokana na maandalizi wanayoendelea kuyafanya.
“Huu ni mchezo wa kuonyesha uimara wetu na hilo sina shaka nalo kutokana na maandalizi tunayofanya katika uwanja wa mazoezi. Al Ahly ni timu bora na ngumu hivyo na sisi tunatakiwa kuwa imara katika kila eneo na hilo nawaahidi mashabiki wetu.
“Hii ni mechi kubwa na ya kihistoria ambayo kama tukipata ushindi itakuwa na maana kubwa kwa timu,” amesema.
Katika nyingine, Robertinho amefurahishwa na urejeo wa nyota wake Henock Inonga na Aishi Manula waliokuwa majeruhi akidai wataongeza kitu katika kikosi chake kutokana na ubora wao.
Manula alikuwa nje akiuguza maumivu ya nyama za paja wakati Inonga alikosa mechi tatu zilizopita za Simba SC kutokana na majeraha ya ugoko.
Wakati huo huo Kikosi cha Simba SC mapema leo Jumamosi (Oktoba 14) kimecheza mchezo wa Kirafiki dhidi ya Dar City FC katika Uwanja wa Mo Simba Arena, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo wa African Football League dhidi ya Al Ahly.
Mchezo huo umeshuhudia Simba SC ikishinda mabao 5-1, yaliyofungwa na Shaban Chilunda aliyefunga mawili, Luis Miquissone, Willy Esomba Onana na Ntobazonkiza.