Rasmi beki wa kati wa Cotton Sports ya nchini Cameroon, Che Fondoh Malone anakuja kuiboresha safu ya ulinzi ya Simba SC katika msimu ujao 2023/24, huku uongozi ukipanga kumtumia mkataba na nyaraka nyingine zote kwa ajili ya kuupitia kabla ya kuusaini.

Mcameroon huyo ni kati ya mabeki wanaotajwa kujiunga na Simba SC katika msimu ujao ambaye anakuja kuchukua nafasi ya Mohammed Outtara aliyevunja mkataba wa miaka miwili.

Simba SC imepanga kuiboresha safu hiyo ya ulinzi ambayo inaongozwa na Hennock Inonga, Joash Onyango na Kennedy Juma anayetajwa kuomba kuondoka kwa mkopo hapo.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Simba SC, kilichobakia kwa kumpata beki huyo ni kumalizana na klabu yake pekee baada ya hivi karibuni kukubali maslahi aliyopewa katika timu hiyo.

Chanzo hicho kimesema kuwa mazungumzo yapo katika hatua za mwisho kati ya Simba na Cotton Sports ambayo ndio inayommliki kuweka ugumu katika kuipata saini yake.

Kiliongeza kuwa kama mazungumzo yatakwenda vizuri, basi uongozi wa Simba utamtumia mkataba beki huyo huko Cameroon kwa ajili ya menejimenti inayomsimamia kuupitia.

“Hakuna shida kwa makubaliano kibinafsi, kwani yalishafanyika siku kadhaa zilizopita, na hakutakuwa na mabadiliko ya bei iliyotajwa mwanzoni ambayo uongozi upo tayari kutoa dau hilo la usajili.

“Hivyo huenda ikakamilisha dili hili kwani tayari mkataba rasmi umeshaandaliwa na nyaraka zote ziko tayari, kilichobakia ni kumtumia kwa ajili ya kuupitia,” kimesema chanzo hicho.

Akizungumzia hilo la usajili, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema: “Kila kitu kinachohusu usajili kipo kwa kocha wetu Robertinho (Roberto Oliviera) ambaye ndiye atasimamia na mara baada ya kukamilika kila kitu tutaweka wazi.”

Buriani Francis Mtega, pole wana-Mbarali
Tushirikiane kulinda vyanzo vya maji - Malisa