Beki wa kati kutoka nchini Cameroon na Klabu ya Simba, Fondoh Che Malone amekiri wapinzani wao Al Ahly ya nchini Misri ni wazuri, lakini haiwafanyi wawaogope watakapokutana.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana Oktoba 20, mwaka huu katika mchezo wa ufunguzi wa michuano ya African Footbal League utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini, Dar es salaam.
Beki huyo alitua Simba SC msimu huu akitokea Cotton Sports ya nchini Cameroon, ambayo iliuza mkataba wake wa mwaka mmoja baada ya kufikia makubaliano.
Che Malone amesema kuwa kila mtu anafahamu ubora wa Al Ahly katika Ukanda wa Afrika, lakini wao kama wachezaji wa Simba SC wana malengo makubwa ya kufika mbali ili waandike historia katika msimu wa kwanza tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo.
“Lipo wazi Al Ahly ni moja ya klabu kubwa na yenye historia katika Ukanda huu wa Afrika, hivyo ni lazima tuiheshimu tutakapokutana nayo katika mchezo wa kwanza tutakaoucheza hapa nyumbani.
“Licha ya ubora wao huo, hautufanyi tuwaogope zaidi ni kuwaheshimu tutakapokutana, na kikubwa tunataka ushindi pekee kwa kuanzia mchezo wa ufunguzi ambao tutacheza Uwanja wa Mkapa.
“Kama beki kila siku naendelea kujifunza kwa kocha wangu katika uwanja wa mazoezi ili kuhakikisha makosa niliyoyafanya katika michezo iliyopita hayajitokezi tena, ili tusiruhusu mabao,” amesema Che Malone