Beki Marcos Alonso amefunguliwa mashtaka na chama cha soka nchini England (FA), kwa tuhuma za kuonyesha mchezo usio wa kiungwana dhidi ya mshambuliaji wa Southampton Shane Long, wakati wa mpambano wa ligi uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita, na The Blues kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.
FA wamemshitaki beki huyo kutoka nchini Hispania, baada ya kufuatilia kosa hilo kwa njia ya picha za televisheni na kuona kuna umuhimu wa kufanya hivyo, kutokana na mwamuzi aliechezesha mtanange huo kutoona madhambi hayo.
Hata hivyo meneja wa Southampton Mark Hughes, ndio alikua chanzo cha kuwashtua FA kufuatia malalamiko yake aliyoyatoa katika mkutano na waandishi wa habari, kwa kusema namna alivyosikitishwa na madhabi aliyofanyiwa mchezaji wake.
Alonso alimsababishia maumivu makali ya kiazi cha mguu Long, baada ya kumchezea ndivyo sivyo, dakika nane kabla ya kipyenga cha mwisho kupulizwa.
Kwa mantiki hiyo huenda Alonso akakosa mchezo wa nusu fainali wa kombe la FA dhidi ya Southampton utakaochezwa Wembley mwishoni mwa juma hili, endapo FA watasisitiza kusikilizwa kwa kesi yake kabla ya mpambano huo wa jumapili.
Alonso ametakiwa kukiria ama kukataa tuhuma hizo kabla ya kesho jumatano saa kumi na mbili jioni kwa saa za England, na kama atakubali tuhuma atafungiwa michezo mitatu.
Mchezo ambayo Alonso yu hatarini kuikosa ni dhidi ya Burnley utakaochezwa keshokutwa Alhamisi, The Saints (Kombe la FA, Jumapili) na Swansea mwishoni mwa juma lijalo.