Klabu ya Chelsea inajiandaa kutuma ofa nyingine kwa ajili ya kiungo Moises Caicedo inayotarajiwa kuwa Pauni 90 milioni kwa mujibu wa ripoti.

Gazeti la SunSports linatambua Mauricio Pochettino ana nia ya kutaka kumnunua kiungo huyo wa kimataifa wa Ecuador anayekipiga Brighton.

Iliripotiwa Brighton inataka Pauni 100 milioni huku ikiwa na matumaini kiungo wake ataanza msimu mpya wa Ligi Kuu England wiki ijayo, lakini Blues imeendela kumkomalia.

Wakati Chelsea ikiwa haijakata tamaa ya kumsajili Caicedo tayari imefanikiwa kunasa saini ya kipa wa Brighton Robers Sanchez kwa Pauni 25 milioni.

Kutokana na uhusiano mzuri na Brighton Blues inaamini uhamisho wa Caicedo kwenda Stamford Bridge ni suala la muda tu na kila kitu kitakamilika.

Ikumbukwe mmiliki wa Chelsea, Todd Boehly alituma ofa tatu Pauni G60 milioni, 70 milioni na 80 milioni hata hivyo zimepigwa chini.

Kwa upande wa Pochettino anaamini kiungo huyo ataongeza nguvu kwenye kikosi chake kutokana na ubora wake alioonyesha tangu alipojiunga na Brighton mwaka 2021 kutoka Independiente del Valle kwa Pauni 3.6 milioni.

Mbali na Caicedo kocha huyo anaiwinda saini ya kiungo wa Southampton mwenye umri wa miaka 19, Romeo Lavia, ambaye anatolewa macho na Liverpool.

Chelsea imebaki na Conor Gallagher, 23, kwenye safu ya kiungo ambaye ni mzoefu baada ya kuwauza N’Golo Kante, Ruben Loftus-Cheek, Matteo Kovacic na Mason Mount kwenye dirisha hili la usajili.

Timu hiyo ya darajani imepewa nafasi kubwa ya kumsajili Caicedo kwa sababu aliweka wazi nia yake ya kutaka kuondoka Brighton.

Naye Kocha wa Brighton, Roberto De Zerbi aliwahi kusema msimu uliopita kwamba kiungo huyo anastahili kucheza soka la kimataifa zaidi lakini mmiliki wa klabu hiyo Tony Bloom hataki kumuachia kizembe kwani nao wanahitaji kuziba pengo lake.

Upatikaji wa Dola: Serikali iongeze jitihada - TAOMAC
Wamiliki Makao ya Watoto zingatieni Sheria - Dkt. Gwajima