Imefahamika kuwa klabu ya Chelsea inaweza kufufua matumaini ya kumsajili Mshambuliaji kutoka nchini Brazil na Klabu Bingwa Ufaransa Paris Saint-Germain, Neymar mwishoni mwa msimu huu 2022/23.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, ambaye alijiunga na kikosi cha PSG mwaka 2017 kwa dau la dunia la pauni mil 200 akitokea FC Barcelona, amekuwa sehemu muhimu ya timu hiyo ya jijini Paris kushinda mataji manne ya ligi katika kipindi hicho.

Kwa mujibu wa Gazeti la Mirror, Rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi anatazamiwa kusimamia mabadiliko ya kikosini humo kwa kuwapiga bei baadhi ya mastaa wa kikosi cha kwanza ili kuhakikisha anatimiza ndoto za kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Ripoti zinadai mmiliki wa Chelsea, Todd Boehly alifanya mkutano mwezi Februari ili kuchunguza upatikanaji wa Neymar na The Blues wanaweza kufufua nia yao.

PSG wanaweza kumuuza Neymar kutokana na kukumbwa na majeraha mara kwa mara huku akilipwa mshahara mkubwa.

Msimu huu kwa Neymar ulimalizika kwa jeraha la kifundo cha mguu mwezi Februari baada ya kufunga mabao 18 na kutoa asisti 17 katika michezo 29.

Kocha Namungo FC afurahia mabadiliko ya ratiba Ligi Kuu
FC Barcelona yalamba €‎ Bilioni 1.5