Vinara wa ligi kuu ya soka nchini England Chelsea, wapo tayari kumuuza mshambuliaji wao Diego Costa mwishoni mwa msimu huu, ili kutimiza lengo la kuwasajili washambuliaji Romelu Lukaku na Alvaro Morata.

The Blues amebadili mawazo na kumuweka kwenye orodha ya wachezaji watakaouzwa mwishoni mwa msimu huu mshambuliaji huyo, baada ya kukataa ofa iliyotumwa na moja ya klabu za nchini China mwezi Januari.

Meneja wa Chelsea Antonio Conte anatajwa kuongoza mpango wa kuuzwa kwa mshambuliaji huyo, ili kufanikisha harakati za upatikanaji wa pesa ambazo zitatumika kuwasajili Lukaku na Morata.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la SunSport umebaini kuwa, tayari mkurugenzi wa ufundi wa Chelsea Michael Emenalo, ameshakubaliana na wazo hilo, na kinachosubiriwa ni kufika mwishoni mwa msimu huu.

Emenalo anaamini Chelsea watakua na nafasi kubwa ya kumsajili tena Lukaku, baada ya kumruhusu kuondoka moja kwa moja mwaka 2014 na kujiunga na Everton.

Kiasi cha Pauni milioni 60 kinakadiriwa kuwa thamani ya usajili wa mshambuliaji huyo kutoka nchini Ubelgiji, huku Morata akifanyiwa tathmini na kuonekana huenda ada yake ya usajili ukafikia Pauni milioni 35.

Medhi Benatia: Ninataka Kucheza Kikosi Cha Kwanza
Ni Zamu Ya Ligi ya Europa kutimua tena