Kikosi cha Antonio Conte (Chelsea) kitakosa posho ya Pauni milioni nne endapo kitapoteza mchezo wa nusu fainali ya kombe la FA dhidi ya Tottenham Hospurs mwishoni mwa juma hili.
Uongozi wa Chelsea umewatahadharisha wachezaji wote wa kikosi cha kwanza kuhusu utaratibu huo, kwa kuamini njia hiyo huenda ikawa sahihi kwa kila mmoja wao kujituma ili kufikia lengo la kucheza mchezo wa fainali wa kombe la FA mwezi ujao.
Tahadhari ya kunyimwa posho kwa wachezaji wa The Blues imetolewa huku wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa ligi dhidi ya Man Utd mwishoni mwa juma lililopita, kwa kukubali kichapo cha mabao mawili kwa sifuri.
Kwa upande wa wachezaji wa Spurs wameahidiwa posho ya Pauni milioni moja, endapo wataifunga Chelsea katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la FA.
Mchezo dhidi ya Tottenham Hotspurs, unapewa uzito mkubwa huko Stamford Bridge kutokana na wanakskazini hao wa jiji la London, kuwa na upinzani mkubwa dhidi ya Chelsea kwa msimu huu.
Katika msimamo wa ligi ya England, Spurs wanashika nafasi ya pili kwa tofauti ya point tano dhidi ya Chelsea walio kileleni, na endapo watafungwa jumamosi, inaaminiwa huenda morari ya wachezaji ikaendelea kushuka na kujikuta wakipoteza matumaini ya kusaka taji la PL.