Klabu ya Chelsea imepania kuzipiku Manchester United na Paris Saint-Germain katika mbio za kuwania saini ya Mshambuliaji wa SSC Napoli, Victor Osimhen, huku ripoti zikisema ipo siriazi na mpango huo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 amewavutia mashabiki wengi Ulaya kutokana na kiwango chake bora alichoonyesha Serie A msimu uliopita alikofunga mabao 26 katika mechi 32 za ligi na kuisaidia SSC Napoli kushinda ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 33.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Nigeria ni moto wa kuotea mbali, na baada ya kusajiliwa na klabu hiyo mwaka 2020 akitokea Lille kwa Pauni 74 milioni, Osimhen ameendelea kuongeza thamani yake huku United ikiripotiwa inajiadaa kutoa Pauni 130 milioni kwa ajili yake.
Gazeti la Mail Sport linatambua kwamba PSG haipo nyuma ikijiandaa kutoa ofa kwa ajili ya straika huyo lakini Chelsea haitakubali kumpoteza kwenye dirisha hili la kiangazi.
Mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Sky Sports, Massimo Marianella amefichua kwamba uongozi wa Chelsea ambayo inanolewa na Mauricio Pochettino unajiandaa kuwasiliana na Napoli kwa simu ili kuweke mambo sawa.
“Taarifa zimeripoti Chelsea wanajiandaa kuwasiliana na Napoli kwa ajili ya uhamisho wa Osimhen,” mwandishi huyo alizungumza kupitia kutuo cha televisheni cha Sky Sports kutoka Italia.
Mwandishi huyo alieleza: “Kwa sasa inaonekana kama mlango mmoja umefungwa. Real Madrid ilihusishwa lakini ikapotezea. Sasa katika mbio hizi timu zilizobaki ni Chelsea, Man United na PSG.”
Hivi karibuni Napoli ilijaribu kumshawishi Osimhen aongeze mkataba mpya kwani mkataba wake wa awali utamalizika 2025.