Klabu ya Chelsea imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuitandika bao 1-0 Mabingwa wa Ligi Kuu England Manchester City katika fainali uliyopigwa Leo Jumamosi Mei 29 katika dimba la Stadio do Dragao lililopo Jijini Porto nchini Ureno.

Ubingwa wa Chelsea umeletwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya benchi la ufundi kutoka timu kuwa chini ya kocha Frank Lampard na sasa Thomas Tuchel aliyeonyesha uhai mpaka msimu unamalizika akiwa na nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya pamoja na ubingwa wa Leo.

Chelsea walikuwa hawapigiwi upatu kubeba taji la Ulaya kuanzia mwanzoni hata ilipobainika kuwa watacheza na Man City fainali bado, nafasi kubwa ilikuwa inaenda kwa Pep Guardiola na kikosi chake.

Tuchel amewaduwaza wapenzi wa kandanda kwa kuendelea kuwa mtawala wa kimbinu kwa Pep Guardiola ukiwa ni mchezo wa tatu kufungwa msimu huu baada ya nusu fainali ya Kombe la FA, Ligi Kuu England na sasa mchezo muhimu wa UEFA.

Bao pekee kwenye mchezo huo limefungwa na kiungo mshambuliaji ghali wa Kijerumani Kai Havertz ungwe ya kwanza akimalizia pasi murua ya Mason Mount lililodumu kwa muda wote wa dakika tisini.

Unakuwa ubingwa wa kwanza kwa kocha Thomas Tuchel, na zaidi ya asilimia 90 ya wachezaji wa kikosi cha Chelsea pia ni ubingwa wao wa kwanza.

ECOWAS kujadili mzozo wa Mali
Rais Samia afanya uteuzi wa Makatibu Tawala wa Mikoa