Imefahamika kuwa Uongozi wa Klabu ya Chelsea upo katika mazungumzo ya siri na Meneja wa Sporting Lisbon ya Ureno Ruben Amorim, ili kufanikiwa lengo la kumkabidhi jukumu la kuliongoza Benchi la Ufundi klabuni hapo msimu ujao wa 2023/24.
Taarifa kutoka jijini London zinaeleza kuwa, Mazungumzo hayo yameanza kufuatia Uongozi wa Chelsea kukoshwa na kiwango cha ukufunzi cha Amorim.
Amorim amekuwa na mwendelezo mzuri katika kikosi cha Sporting Lisbon baada ya kuingoza timu hiyo kufanya vizuri kwenye Michuano ya Europa League wakiwa hatua ya Robo Fainali na wakiwa na kumbukumbu ya kuwachapa Arsenal kwenye kombe hilo.
Meneja huyo anatabiriwa huenda akachukua mikoba ya Graham Potter ambaye alifukuzwa ndani ya timu hiyo kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo, lakini nafasi yake kwa sasa inakaimiwa na Frank Lampard hadi mwishoni mwa msimu huu 2022/23.
Licha ya Meneja huyo kupewa asilimia kubwa za kuichukua timu hiyo, mmiliki wa Chelsea, Todd Boehly amekuwa akifanya mawasiliano na Mameneja wengine kama Luis Enrique, Julien Nagelsmann na Marco Silva kwa ajili ya kubeba mikoba hiyo.
Kylian Mbappe aweka rekodi Paris Saint-Germain
Amorim mwenye umri wa miaka 38, amekuwa na misimu bora ndani ya Sporting akiifanya timu hiyo kutwaa taji la Ligi Kuu Ureno kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 19, huku pia akichukua mataji mengine matatu ya nchi hiyo.