Klabu ya Uingereza, Chelsea imefanikiwa kumsajili mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Christian Pulisic kwa kitita cha Euro 64 Milioni, sawa na $73.1 Milioni.
Chelsea imekamilisha hatua hiyo lakini imewapa wapiga soka hao wa Bundesliga awachezee kwa mkopo katika kipindi cha msimu huu kabla hajahamia rasmi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza msimu ujao wa kiangazi.
Klabu hiyo ya Uingereza imemnasa mchezaji huyo machachari mwenye umri wa miaka 20 kabla ya kukamilisha hatma ya mkataba wake na Dortmund uliokuwa ukamilike mwaka 2020.
“Ilikuwa ni ndoto ya muda mrefu wa Christian kucheza Ligi Kuu ya Uingereza. Hayo yalikuwa matakwa ya mchezaji huyu wa Marekani kwa muda mrefu, hivyo sisi hatukuweza kuongeza muda wa mkataba wake,” amesema Mkurugenzi wa michezo wa Dortmund, Michael Zorc.
Vyanzo vya ndani vya timu hizo vimekaririwa vikieleza kuwa baada ya kipindi cha miezi sita, mchezaji huyo ataruhusiwa kuanza kuitumikia Chelsea.
Christian alijiunga na Dortmund kama kijana mdogo mwaka 2015, mbio za uwanjani zilizoanza mwaka 2016 zilimpa nafasi ya kushiriki mechi nyingi. Ameichezea timu hiyo katika misimu minne na kuwa katika sehemu ya kikosi kilichotwaa kombe la Ujerumani mwaka 2017.
Akiwa na timu yake ya Taifa ya Marekani, alifanikiwa kuifungia magoli 9 kati ya michezo 23 aliyoshiriki.