Klabu ya Chelsea imemuadhibu Kepa Arrizabalaga aliyemgomea kocha Maurizio Sarri alipotaka ampishe golikipa mwenzake, Willy Caballero katika muda wa mikwaju ya penati dhidi ya Manchester City.
Katika mchezo huo, Arrizabalaga alianguka chini dakika za mwisho na kuonesha kuwa amejeruhiwa, kitendo kilichomfanya Sarri kuamua kumbadilisha na kumuweka Caballero ambaye ana historia nzuri zaidi ya kuzuia mikwaju ya penati.
Hata hivyo, Arrizabalaga alimgomea kocha huyo licha ya kuwekewa msisitizo. Sarri alionekana kuchukizwa na kitendo kile huku akitamani kupiga kila kilichokuwa mbele yake.
Matokeo ya mikwaju hiyo yaliyoshuhudiwa Chelsea ikipoteza 4-3 dhidi ya Manchester City yalikuwa maumivu mengine yaliyochochewa na mzozo huo.
Chelsea imetoa taarifa yake kwa vyombo vya habari Jana usiku, ikieleza kuwa golikipa huyo mwenye umri wa miaka 24 ataadhibiwa kwa kulipa faini ya kiasi cha mshahara wake wa wiki moja.
Aidha, Arrizabalaga aliomba radhi kwa kitendo hicho na kueleza kuwa atatumikia adhabu yoyote atakayopewa na timu yake.
“Ninaomba kuchukua nafasi hii kumuomba radhi kocha, Willy na wachezaji wenzangu pamoja na klabu kwa ujumla. Nilifanya haya na sasa ninataka kuwaomba radhi pia mashabiki,” alisema Arrizabalaga.
“Nimejifunza kutokana na kitendo hiki na ninakubaliana na adhabu yoyote kama ambavyo klabu itaamua,” aliongeza.
Naye Kocha Sarri alieleza kuwa alizungumza na golikipa huyo na kwamba alikiri kufanya makosa makubwa na kwamba hatarudia. Amesema uhusiano kati yao uko vizuri kwani ilikuwa hali ya kutoelewana tu.