Mkurugenzi Mtendaji wa Inter Milan, Beppe Marotta, ameionya Chelsea kwamba haiwezi kudai ada kubwa ili kuachana na mshambuliaji wao, Romelu Lukaku.
Lukaku amerejea Chelsea baada ya mkopo wake na Inter kuisha na pande zote tatu zinataka kufikia makubaliano ambayo yatamfanya Mshambuliaji huyo kutoka nchini Ubelgiji kusalia na ‘The Nerazzurri’ kwa mwaka ujao na zaidi.
Chelsea imekataa ofa ya mkopo wa moja kwa moja kutoka Inter Milan na badala yake inashinikiza kuuzwa kwa mkataba kudumu msimu huu wa majira ya joto, ingawa maelewano yanaweza kufikiwa juu ya dau la mkopo na jukumu la Inter kumnunua Lukaku msimu wa 2024.
Vyovyote itakavyokuwa, Chelsea wanajiandaa kubeba hasara kubwa kwa Lukaku, ambaye aliigharimu Pauni milioni 97.5 alipojiunga nayo mwaka 2021.
“Kwa Lukaku, Chelsea italazimika kutathmini kama anafanya kazi katika mradi wao; kama hafanyi hivyo, mikakati yao inabadilika,” amesema Marotta akiiambia Sky Italia.
“Ni wazi kuwa hawawezi kufikiria kumweka sokoni na kupokea ofa muhimu.
“Siyo bahati mbaya kwamba uwezekano wa mauzo kwa Saudi Arabia ulikuwa karibu Euro milioni 50. Hiyo inaweza kuwa lengo ambalo ni mbali sana na Euro milioni 115 tulizoomba, na kupata, kumuuza miaka miwili iliyopita.”
Lukaku aliichezea Chelsea mechi 44 katika msimu wake wa kwanza akiwa Stamford Bridge, lakini alichangia mabao 15 pekee na alidai kuwa anataka kurejea Inter miezi michache tu baada ya kuondoka.
Alitumia msimu uliopita kwa mkopo na Inter na Chelsea wako tayari kukata uhusiano wa kudumu msimu huu wa majira ya joto.
‘The Blues’ walijaribu kumuuza Lukaku Saudi Arabia, lakini alikataa ofa hiyo, akisisitiza nia ya kurejea Inter Milan.
Msimamo huo umeongeza nia ya Inter kuungana tena na Lukaku, lakini wasiwasi wa kifedha wa Nerazzurri umefanya mazungumzo kuwa magumu hadi sasa. Hata hivyo, pamoja na kila mtu kufanya kazi kwa lengo moja, maelewano yanatarajiwa kufikiwa hivi karibuni.