Mshambuliaji wa klabu ya Fluminense, Robert Kenedy Nunes do Nascimento, jana jioni alifanyiwa vipimo vya afya huko jijini London, ikiwa ni sehemu ya kukamilisha usajili wa kujiunga na klabu bingwa ya Uingereza, Chelsea kwa ada ya uhamisho wa paund milioni 6.3.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 19, alikuwa kwenye mipango ya kuelekea jijini London kukamilisha uhamisho wake tangu majuma mawili yaliyopita baada ya viongozi wa klabu ya Fluminense kumaliza mazungumzo na viongozi wa Chelsea.
Kenedy, atakuwa mchezaji wa pili kusajili huko Stamford Bridge akitokea nchini Brazil kwa mwaka huu, baada ya usajili wa Nathan aliyekuwa akiitumikia klabu ya Atletico Paranaense mwezi Mei.

Hata hivyo, Kenedy alikuwa akifuatiliwa kwa ukaribu na klabu kubwa barani Ulaya kama Manchester United, Barcelona, Juventus pamoja na Wolfsburg ya Ujerumani, lakini Chelsea wametumia mbinu zao na kufanikiwa kumnasa.
Mshambuliaji huyo ni miongoni mwa wachezaji wanaocheza katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil chini ya umri wa miaka 20.

Serena Aendelea 'Kuchachafya' Jijini London
Uongozi Wa Wembley Wakanusha Kupokea Ofa Ya Chelsea